Jumapili, 22 Juni 2014

NADHARIA ZA MAANA




NADHARIA KATIKA SEMANTIKI

Kutokana na ugumu wa kufasili maana ya maana katika taaluma ya semantiki ambayo ni tawi la isimu ambalo hujihusisha na uchunguzi wa lugha katika maana hususani maana ya msingi, taaluma hii hushughulikia maana za maneno na sentensi katika lugha mahususi na maana hizo hushughulikiwa kisayansi.

Maana katika semantiki ilianzakushughulikiwa tangu enzi za Plato, Aristotle, wataalamu mbalimbali walishughulikia falsafa, mantiki, saikolojia, isimu na Athropolojia. Kila taaluma ilitofautiana, kulikuwa na tofauti ya isimu na taaluma nyingine. Tofauti ya isimu na taaluma nyingine ni kwamba isimu iliangalia maana kisayansi na usayansi huo ulikuwa wa kiupangilifu, kiuakinifu kwa kutumia kanuni mbalimbali, ingawa walitumia kanuni bado kulikuwa na matatizo mbalimbali.

Swali
Kwa nini bado kulikuwa na matatizo ya kufasili maana ya maana?

Jibu: maana ilichukuliwa kama kitu ambacho akijatengamaa na kilikuwa tepetepe ama telezi kwani huwezi kukishika, kinateleza. Mfano maji huchukuliwa katika kikombe na maana hasa hutegemea sana uwezo na ufafanuzi wa msemaji kwa mantiki hiyo maana hufananishwa na kinyonga, maana hutegemea muktadha wa mzungumzaji. Wanahisimu wanaona kuwa maana ni kitu muhimu katika mawasiliano na maana inapokuwa tege mawasiliano huwa si kamili na hakika mawasiliano bila maana si kitu. Kwa maana hiyo maana ni muhimu sana katika mawasiliano kwani kuna kuwa na kitu ambacho mzungumzaji amekusudia kukisema.

Maana ya maana
Habwe na Karanja (2007), wanasema neno maana lina fahiwa nyingi watu wa kawaida wamelitumia kumaanisha vitu mbalimbali.
Mfano i/ una maana gani kufika umechelewa?,



ii/ yale mawingu meusi yana maana mvua itanyesha sasa,
iii/ mtu huyu hana maana yoyote,
iv/ manyunyu ina maana, mvua inayonyesha kidogokidogo,
v/ kuna joto,
vi/ kicheko katika mashetani kina maana gani?,
vii/ Aota maana yake ni mshipa mkubwa utokao moyoni na kupeleka damu sehemu za mwili,
viii/ msaada wako una maana sana kwetu. Sentensi hizi zina maana mbalimbali kama vile sababu, dalili, ishara, hafai, ufafanuzi, hali, kejeli, umuhimu. Swali katika tungo hizo ni maana ipi inayohusu maana ya msingi katika muktadha wa semantiki. Matumizi mapana na hivyo ni tata ili kuweka mipaka ya semantiki ni muhimu kubainisha maana ya maana ya semantiki.

Kutokana na utata wa maana kuliibua nadharia mbalimbali ambazo kwa kiasi fulani zimejikita katika kupunguza utata huo wa kuelezea maana ya maana. Katika mjadala huu nadharia bainishi kama vile urejeleo, nadharia tumizi, taswira/dhana, vichocheo mwitikio, vijenzi semantiki.

UREJELEO
Nadharia hii iliasisiwa na Ogden, C.K na Richards, I. A. Nadharia hii inahusu uhusiano baina ya kiambo cha lugha na kitu au vitu katika ulimwengu wa masilugha. Kwa mtazamo huu maana ya neno ni kitu halisi kinachorejerewa na neno. Maneno ni majina ambayo dhima yake ni kutaja vitu. Maana ya neno ni uhusiano baina ya neno hilo na kitu au vitu ambavyo neno hilo hurejelewa. Kwa mfano, kitabu, simu n.k.



UPUNGUFU
i/ si kilia kiambo au leksimu yenye maana ina kirejerewa chake. Mfano, katika lugha
   kuna vinyambo ambavyo havina kirejeleo. Kama vile Mungu, upepo, shetani, (dhana).


ii/ haifanyi kazi kwa maneno yenye uhusiano wa kipolisemia. Kwa mfano Kichwa ni
    leksimu yenye kuchanuza maana nyingi.

iii/ Haifanyi kazi kwa maneno yenye uhusiano wa kihomonomia. Kama vile kaa, chunga,
     chungu, n.k.

iv/ pia haiwezi kufanya kazi katika maneno yenye uhusiano wa kisinonimia, vinyambo
     zaidi ya kimoja (kisawe).

NADHARIA YA DHANA / TASWIRA
Nadharia hii inafafanua kuwa maneno ya kiambo ni dhana au taswira inayoibiliwa na kiambo hicho akilini mwa mwanalugha pindi kiambo hicho kinapotumika.
Neno – kisemo- sentensi, kisemo ni dhana ijengekayo akilini mara tu msemaji au msikilizaji anapozungumza ama kusikiliza, pia nadharia hii uhusisha maana na wazo, uhusisha maana na kitu moja kwa moja hivyo inasaidia kutoa majibu ya vinyambo visivyoweza kurejelewa.

MAPUNGUFU
·         Si bainifu na haiwezi kuchunguzika, kutabili chochote, mwanaisimu hawezi kufanya utafiti wa aina moja.
·         Picha za akilini ni dhahania ya kutosha kuweza kuwakilisha maana za nomino au vitenzi vya kawaida.
·         Hakuna picha za jumla ya mguso.
·         Si kila kiambo kinahusiana na taswira.
·         Haiwezi kuelezea viambo viwili kuwa ni kisawe. Kinyambo huwa na taswira moja haina visawe.
·         Haiwezi kuelezea maana ya sentensi au nahau.

NADHARIA TUMIZI
Nadharia hii iliasisiwa na mwanafalsafa mashuhuri aliyejulikana kwa jina la Ludwing Wittgenstein mwaka 1930, alitamka kwa mifano mingi ya maneno kuwa maana ya


neno ni matumizi yake katika lugha, msisitizo wake upo katika maana ya neno au kisemo kilichotumika katika muktadha maalumu. Mtaalamu huyu anaona kuwa maana ya neno ni matokeo au athari inayotokana na matumizi. Hata hivyo si muhimu kuuliza maana ya neno bali matumizi yake katika muktadha husika.
Nadharia hii imepunguza matatizo katika nadharia tangulizi kwani watoto wanapojifunza lugha hujifunza maana ya viambo vya lugha kutokana na jinsi vinyambo hivyo vinavyotumika na wanalugha wa jamii.
NADHARIA NA MATATIZO
Ø  Si kweli kuwa maana ya matumizi ya neno hupatikana katika matumizi ya neno,
Ø  Inahalalisha tabia ya mabadiliko ya maana kutokana na muktadha.
Ø  Huifanya maana iwe mali ya kundi fulani.

NADHARIA YA VICHOCHEO MWITIKO
Nadharia hii iliasisiwa na mtaalamu ajulikanaye kwa jina la Bloomfield 1933, nadharia hii imejikita hasa katika kuchunguza maana ya umbo la kiisimu na hali ambamo msemaji hutamka umbo hilo na mwitiko huibuliwa na msikilizaji. Maana ni kichocheo cha msemaji na mwitiko wa msikilizaji. Mtaalamu huyu anadai kuwa maana ya kisemo huwa katika muundo wa tendo uneni.
CHOCHEO →MWITIKO………CHOCHEO → MWITIKO
Kasekwa anaumwa njaa, anaona tofaa mtini(hali ya msemaji) anatamka kuwa anataka tofaa (mwitiko wa msemaji)
          NJAA                                               ANATAKA
             ↓                                                             ↓
       CHOCHEO                                           MWITIKO
Kapele anachochewa kuitika kwa kuruka ua, anaruka ua anapanda mti anachuma embe na kuliweka mikononi mwa kasekwa.
CHOCHEO → MWITIKO
NJAA   → NATAKA
CHAKULA → KUPOKEA



Matatizo ya nadharia
v  Unaweza kueleza maana chache za kisemo cha lugha kwa kuwa hali nyingi za matumizi zimechanganyikana, semo nyingi za lugha hazithibitiwi na kichocheo katika muktadha zitokanamo. Kwa mfano mtu akiulizwa swali si lazima atoe jibu.
v  Maneno mengi hayataji vitu vionekanavyo au nduni zionekanazo , mfano njaa.
v  Wanalugha hawapokei maneno kwa vitu vinavyowakilisha maneno hayo.
v  Maneno dhahania hayaelezeki katika nadharia hii. Mfano njaa.


VIJENZI SEMANTIKI
Hudai kuwa leksimu zote zaweza kuchanganuliwa kwa kuzingatia seti si ukomo ya vijenzi semantiki ambavyo ni jumla. (Crystal, 1969) uchanganuzi wa vijenzi semantiki ni mkabala uanochunguza leksimu tu. Mfano mwanamke, fahiwa ya leksimu hii ina vijenzi vitatu ambavyo kwa hakika ni;
                                            i.            Mtu
                                          ii.            Mtu mzima
                                        iii.            me
                    Ufafanuzi
        i.            MWANAMKE = [+MTU], [+MTU MZIMA], [-ME]
      ii.            MSICHANA = [+MTU], [-MTU MZIMA], [-ME]
    iii.            MWANAMUME = [+MTU], [+MTU MZIMA], [+ME]
Kadhalika vijenzi semantiki huwa na jozi kinzani, jozi hizo huoneshwa kwa alama ya toa na jumlisha. Kijenzi mtu ni cha jimla kinahusisha leksimu hiyo na leksimu kinzani. Leksimu kinzani, mti, majani, vijenzi semantiki vya kijumla kama [MTU], [KITU], [OEVU] n.k. hutumika kupambanua leksimu zilizo katika makundi tofautitofauti ya maana. Dhima kuu ya vijenzi semantiki ni kupambanua leksimu zilizo katika kikoa kimoja cha maana. Kijenzi semantiki [ME] na [MTU MZIMA] tunaweza kufafanua maana za mwanamke, mwanamume, mvulana pamoja na msichana maneno haya ni vikoa vya maneno sawa.
Kwa mfano;

MWANAMKE
a.       MWANAMKE  [- ME], [+MTU MZIMA]
b.      MWANAUME [+ME], [+MTU MZIMA]
c.       MVULANA [+ME], [-MTU MZIMA]
d.      MSICHANA [-ME], [-MTU MZIMA]
     Upambanuzi huu unaonesha kuwa leksimu mwanamke inatofautiana na leksimu mwanamume kwa kutoa [-ME], leksimu msichana inatofautiana na leksimu mvulana kwa kutoa alama [-ME], pia leksimu mvulana inatofautiana na leksimu msichana kwa kujumlisha [+ME]
Mfano undugu wa damu.
Baba
Mama

Shangazi
Mjomba

Kaka
Dada

Mwana
Binti

Mpwa
Binamu

Maneno haya ya udugu wa damu ni tofauti na maneno mengine kwa kuwa yenyewe yanarejelewa kiwakilishi cha msemaji. Maneno hayo yanaweza kuwakilishwa kwa kijenzi kimoja ndugu na ili kukitofautisha ni lazima kiwe na kijenzi kingine.

Kwa mfano
                 [+me], [+mzazi], [mlalo],   [mfuatano]
Baba         [+me], [+mzazi], [-mlalo], [-mfuatano]
Mama       [-me], [+mzazi], [-mlalo], [-mfuatano]
Shangazi   [-me], [-mzazi], [-mlalo], [-mfuatano]
Mjomba    [+me], [-mzazi], [-mlalo], [-mfuatano]
Kaka         [+me], [-mzazi], [+mlalo], [+mfuatano]
Dada         [-me], [-mzazi], [+mlalo], [+mfuatano]
Binti         [-me], [-mzazi], [-mlamlo], [-mfuatano]
Mwana     [+me], [-mzazi], [-mlalo], [-mfuatano]
Mpwa       [-/+me], [-mzazi], [-mlalo], [-mfuatano]
Binamu     [-/+me], [mzazi], [-mlalo], [-mfuatano]



ULALO ngazi ya uhusiano wa usawa.
MFUATANO uhusiano wa wima.

Swali muhimu
Jadili ugumu unaojitokeza katika kufasili maana ya maana kwa kuzingatia nadharia za maana.


MAPUNGUFU YA KIJENZI SEMANTIKI
                                i.            Kutokuwepo kwa vijenzi vya uteuzi wa vijenzi, kwa hawajaeleza wazi ni kwanini wanatumia me na ke, kijenzi mlalo, na wima na si vinginevyo. Mzazi na mafuatano. Hivyo ni muhimu kueleza kwanini vigezo hivyo vimetumika.
                              ii.            Mkabala huu unatumia mbinu ya uwili ukinzani ambao unawakilishwa na alama za kujumlisha na kutoa. Unaweza kufaa kwa leksimu ambazo vijenzi vyake vinaweza kubainika kwa urahisi. Lakini pia unweza kufaa Zaidi katika leksimu nyingine kama vile viwakilishi.
                            iii.            Hakuna kikoa cha vijenzi semantiki hivyo hakuna kigezo maalumu kinachoweza kueleza idadi ya vijenzi semantiki.




   


  

Maoni 13 :

  1. Asante sana kwa matihi haya ambayo yanamsaidia msomaji kuelewa maana ya maana na nadharia. lakini nivema mnapoandika matini za kitaaluma muambatanishe au muweke marejeleo mwishoni ilikumuwezesha msomaji kujua ni wapi na kwavipi atapata ufafanuzi zaidi juu ya kilichojadiliwa katika matini na kujiridhisha. ahsante sana.

    JibuFuta
  2. kazi nzuri.Ningependa mnijulishe umuhimu wa semantiki katika uchambuzi wa Isimu

    JibuFuta
  3. Ahsante sana. Naomba Nielezwe Umuhimu was Semantiki katika kutekeleza Majukumu.

    JibuFuta
  4. Naomba historia ya semantiki

    JibuFuta
  5. Sababu zipi zinachangia mabadiliko ya maana katika lugha?

    JibuFuta
  6. Kazi nzuri lakini naomba kujua mabadiliko ya semantiki katika lugha

    JibuFuta
  7. Ni zipi hatua za utokeaji wa kitendo uneni

    JibuFuta
  8. Marejeo ni muhimu katika kazi ya kitaaluma.

    JibuFuta
  9. Nini maana ya taaswira

    JibuFuta
  10. Kazi kuntu jamani,,,mmenisaidia sana

    JibuFuta